📖 Story Tamu

Episode 8: KILELE CHA AGANO LA DAMU

Mvua haikunyesha, lakini hewa ilijaa harufu ya vumbi na kitu kinachoungua. Yule mzee aliyesimama juu ya mlima wa takataka alicheka kicheko kilichopasua ngoma za masikio yetu. Kila alipogonga fimbo yake chini, ardhi ya lile jalala ilitetemeka.

"Juma! Ulikuja kwangu ukiwa unalia, huna hata ndala miguuni! Nikakupa kila kitu, nikakupa heshima ya mjini! Leo unaniletea mwanga mweupe kwenye ardhi yangu?" Sauti ya yule mganga ilikuwa kama mngurumo wa simba aliyejeruhiwa.

Juma alikuwa akitapa chini ya yale mabati, akijaribu kuficha uso wake. "Nisamehe babu! Sikuleta mimi, huyu mwanamke alikuja mwenyewe! Chukuat kila kitu, chukua hata uhai wangu lakini usiniue kwa mateso haya!"

Mganga aligeuza macho yake yaliyokuwa mekundu kama mkaa uliokolea moto na kunitazama mimi, kisha akamtazama Neema aliyekuwa akigaagaa kwa uchungu kwenye gari la polisi. Polisi wale, ambao mwanzo walionekana kuwa na ujasiri, walikuwa wameparalaiti; walisimama kama masanamu, macho yao yakiwa wazi lakini hawawezi hata kupepesa.

"Wewe mgeni!" Mganga alininyooshea fimbo yake. "Huyu mwanamke amebeba kiumbe ambacho hakitakiwi kuwepo kwenye agano langu. Damu ya huyo mtoto ni sumu kwa mali zangu. Ni lazima mmoja wenu afe hapa leo ili mizimu itulie!"

Nilihisi baridi kali ikipanda kutoka miguuni kuelekea moyoni. Lakini ajabu ni kwamba, kadiri yule mganga alivyozidi kusogea, ndivyo ule mwanga kutoka tumboni mwa Neema ulivyozidi kuwa mkali. Haikuwa mwanga wa kawaida; ulikuwa ni mwanga uliokuwa unatoa joto la amani, ukipingana na baridi ya kishirikina ya yule mzee.

"Neema, kaza moyo!" Nilipiga kelele, nikijaribu kuvunja ule ukuta wa hofu.

Mganga alikasirika. Alirusha fimbo yake hewani, na ghafla maelfu ya wale wadudu weusi (mende wa ajabu) walifurika kutoka kila upande wakituelekea. Walikuwa wakitoa sauti ya kutisha ya kukwangua miamba.

"Leo ndiyo mwisho wa ukoo wako, Juma!" Mganga alipiga yowe.

Lakini kabla wadudu wale hawajatufikia, Neema alitoa ukelele mmoja mrefu wa mwisho, na ghafla... *PAAAA!* Kitu kama radi ndogo ilitokea pale alipokaa Neema. Mwanga ule ulilipuka na kusambaa kama wimbi la bahari. Kila mdudu aliyeguswa na mwanga ule aligeuka kuwa jivu papo hapo. Yule mganga alirushwa nyuma na kuanguka kutoka juu ya ule mlima wa takataka.

Ule ukimya wa kutisha ulitoweka. Polisi walizinduka na kuanza kukohoa, wakishangaa nini kimetokea. Nilimkimbilia Neema na kumkuta akiwa ametulia, jasho likimtiririka, lakini hakuwa na maumivu tena.

"Mtoto... mtoto yuko wapi?" Niliuliza kwa hofu.

Neema alitazama tumbo lake; lilikuwa limepungua, lakini hakukuwa na mtoto aliyezaliwa. "Hawezi kuzaliwa hapa," Neema alinong'ona kwa sauti ya kimalaika. "Amesharudisha giza kule lilipotoka, sasa ni wakati wa kuondoka."

Nilikimbia kule alipokuwa Juma. Nilimkuta bado amelala, lakini safari hii alikuwa ametulia. Alinitazama na kutabasamu kidogo, tabasamu la mtu aliyekubali hatima yake.

"Mwanangu... nimeona kila kitu. Mwanga umemshinda giza... lakini mimi siwezi kuondoka nanyi. Mimi ni sehemu ya hili jalala sasa," Juma alisema huku akianza kufifia kama moshi.

"Juma! Usiseme hivyo, twende hospitali!" nililia.

"Huwezi kutibu roho iliyouzwa, rafiki yangu. Mchukue Neema, nenda naye mbali na mji huu. Na usirudi tena kunitafuta. Kumbuka... utajiri wa haraka una masharti ya damu, na damu haishibi kamwe."

Mbele ya macho yangu, Juma aligeuka kuwa rundo la majivu, na upepo mdogo ukayapeperusha majivu yale na kuyachanganya na takataka za lile jalala la kale.

Polisi walitukaribia, wakiwa wamechanganyikiwa. "Jamani, yule mgonjwa yuko wapi? Na yule mzee aliyekuwa juu ya kilima amepotelea wapi?"

Niliwatazama, kisha nikamtazama Neema. "Hakuna mtu hapa. Twende zetu."

Tuliondoka kwenye lile eneo la laana, lakini huku nyuma, kicheko cha yule mganga kiliendelea kusikika kwa mbali, kikirindima kwenye magofu ya utajiri uliopotea.

**Je, Juma amekufa kweli? Na nini hatma ya kile kiumbe ambacho hakikuzaliwa lakini kilishinda giza?**

**Usikose Sehemu ya 9...**
Matangazo
Matangazo