✦ Matangazo ✦

πŸ“– Story Tamu

Episode 4: Sehemu ya 4: Mwaliko wa Usiku

Hassan alizitazama zile picha kwenye gazeti la udaku, akahisi mapigo ya moyo wake yakimwenda mbio. Hakujua kuwa kile kilikuwa ni mwanzo wa dhoruba ambayo angeishindwa kuizuia.

Giza lilipoanza kuingia jijini Mwanza, Hassan alikuwa bado ameketi sebuleni akimsubiri mke wake. Alikuwa ameandaa chakula cha usiku kwa upendoβ€”samaki sato wa kukaanga na ndizi, chakula ambacho Anifa alikuwa akikipenda sana tangu walipokutana.

Lakini saa mbili usiku, mlango ulifunguliwa kwa kishindo. Anifa aliingia akiwa ameambatana na Bi Husna. Walikuwa wakicheka kwa kelele, harufu ya pombe kali ikitangulia kabla yao.

"Mke wangu, umerudi? Karibu chakula, nimepika mpendwa," Hassan alisema akijaribu kutabasamu licha ya maumivu ya moyo.

Anifa alimtazama Hassan kwa jicho la dharau, kisha akatazama meza ya chakula. "Samaki? Kila siku samaki na ndizi? Hassan, kweli wewe ni daktari au ni muuza samaki wa mwaloni? Leo nimekula 'Buffet' ya laki moja kwenye hoteli ya kitalii, unaniletea samaki wako wa mafuta ya kienyeji hapa?"

Bi Husna alicheka kicheko kilekile cha kejeli. "Shoga, mwambie mumeo kuwa leo tuna mwaliko maalum. Kuna 'Party' ya usiku kwenye 'Yacht' ziwani. Matajiri wa madini kutoka Geita wapo mjini, na wanataka kuona warembo wa Mwanza."

Hassan alisimama ghafla. "Mke wangu, huwezi kwenda kwenye pati ya usiku na watu tusiowajua. Wewe ni mke wa mtu, na mimi ni mumeo. Heshima yako ni heshima yangu."

Anifa alimsogelea Hassan mpaka usoni, kidole chake kikimnyooshea. "Heshima gani? Heshima ya kulala njaa? Heshima ya kuvaa nguo za mtumba kisa mume wangu ni daktari maskini? Sikiliza Hassan, kuanzia leo, usipangiwe maisha yangu. Mimi ni mrembo, na uzuri huu unahitaji gharama ambazo wewe huna."

"Anifa, unajua unachokisema?" Hassan aliuliza, sauti yake ikitetemeka kwa uchungu.

"Nakataa kuwa mtumwa wa umaskini wako!" Anifa alifoka. "Husna, twende zetu. Hapa kuna harufu ya umaskini inanichefua."

Anifa aliingia chumbani, akachukua pochi yake ya gharama aliyopewa na Bi Husna kama "ndoano", kisha akatoka nje bila hata kumuangalia Hassan aliyekuwa ameshika kichwa chake.

Hassan alishindwa kustahimili, machozi yalimtoka. Alijaribu kumzuia mlangoni, lakini Bi Husna alimsukuma pembeni. "Kaa mbali daktari, huyu si saizi yako tena. Kamtibie mama yako, Anifa ana wagonjwa wengine wenye mifuko mizito!"

Waliingia kwenye gari la kifahari lililokuwa linasubiri nje, huku muziki mkubwa ukiwa umewashwa. Hassan alibaki amesimama mlangoni, akitazama taa za gari zikipotea gizani. Alirudi ndani na kukaa kwenye sofa, akitazama kile chakula alichopika kwa upendo kikizidi kupoa.

Usiku ule, Anifa alijikuta kwenye ulimwengu mwingine. Mvinyo wa gharama, muziki wa kileo, na wanaume wenye suti za gharama walioanza kumvuta mashati kwa sifa. Alijihisi kama malkia, akisahau kabisa kuwa nyumbani kuna mwanaume aliyemtoa hospitalini na kumpa jina la "Mke".

---
**Je, Anifa atarudi nyumbani usiku huo? Na nini kitatokea atakapokutana na tajiri atakayempa ofa ya kumuacha Hassan jumla? Usikose Sehemu ya 5.**