✦ Matangazo ✦

📖 Story Tamu

Episode 3: Sumu ya Maneno

Hassan alibaki amesimama sebuleni, macho yake yakitazama keki iliyomwagika sakafuni. Moyo wake ulianza kudunda kwa kasi. Hakuelewa ni nini kimetokea kwa Anifa yule mpole aliyemjua hospitalini. Hapa ndipo mwanzo wa dhoruba ilipoanza rasmi.

Siku iliyofuata ilikuwa ya Jumapili, siku ambayo kawaida Hassan na Anifa walikuwa wakishinda pamoja wakipumzika. Lakini asubuhi hiyo, Anifa aliamka na kuanza kujipamba kwa nakshi nyingi kuliko kawaida. Alivaa nguo fupi ya gharama na kupaka marashi yanayovuta hisia kutoka mbali.

"Mke wangu, unakwenda wapi asubuhi hii?" Hassan aliuliza huku akijaribu kutengeneza mazingira ya amani kwa kumletea chai kitandani.

Anifa hakugeuka, aliendelea kujitazama kwenye kioo na kupaka rangi ya mdomo (lipstick) nyekundu iliyokolea. "Naenda kwa Bi Husna. Tuna kikao cha harusi ya shoga yetu mwingine. Naomba laki mbili ya mchango."

Hassan alishusha pumzi ndefu. "Laki mbili? Mbona ghafla mpenzi? Na unajua jana tu nimekupa laki tano ya matumizi ya ndani. Bajeti yetu ya mwezi huu imebana kidogo."

Anifa aligeuka kwa kasi, macho yake yakiwa yamebeba cheche za dharau. "Imebana? Kila siku kwako bajeti imebana! Hivi wewe ni mwanaume wa aina gani? Yaani laki mbili tu unalalamika kama umeombwa kiwanja? Angalia wenzio, wanatoa mamilioni kwa wake zao bila hata kuulizwa. Umeishia kunifungia hapa ndani kwenye nyumba ya kupanga, halafu unataka nikuone shujaa?"

Hassan alijaribu kumsogelea na kumshika mkono. "Anifa mke wangu, tulia. Maisha ni hatua. Mimi ni daktari, nafanya kazi kwa bidii ili baadae tujenge nyumba yetu. Hawa marafiki zako wanakupeleka siko..."

"Niondoe mkono wako!" Anifa alifoka na kumsukuma Hassan kwa nguvu. "Usinitafutie sababu ya ugomvi. Kama huna hela sema, nitajua wapi pa kuipata. Uzuri wangu huu hauwezi kuozea hapa ndani kwa sababu ya bahili kama wewe."

Anifa alitoka nje kwa madaha, akizitupa funguo za nyumba mezani kwa kishindo. Hassan alibaki ameketi kwenye kochi, kichwa kikimuuma. Alihisi kama anapoteza mke wake mbele ya macho yake.

Kule kwa Bi Husna, Anifa alikutana na kundi la wanawake waliokuwa wakiongelea maisha ya anasa pekee. Bi Husna alimkaribisha kwa kicheko cha kejeli.

> "Hee! Shoga angu mbona unanuka harufu ya sabuni ya mche? Yaani Hassan hata marashi ya gharama hawezi kukununulia? Njoo hapa, mimi nina 'baba mwenye nyumba' wangu hapa mjini, anataka mwanamke mrembo kama wewe wa kwenda naye kwenye pati ya usiku wa leo. Utapata hela ambayo Hassan hajawahi kuiona tangu aanze udaktari wake."

Anifa alicheka, moyo wake ukishawishika. "Kweli shoga? Maana huyu dume suruali wangu kashaanza kunichosha na habari zake za kubana matumizi."

Zuhura aliongezea kwa sauti ya juu, "Achana nae huyo! Mwanamke ni sifa, na sifa ni pesa. Leo usiku tutakupeleka ukajue maana ya maisha ya mjini."

Wakati huo huo, Hassan akiwa nyumbani, aliamua kufanya usafi wa ndani ili kumtuliza mke wake akirudi. Wakati akifanya usafi chini ya kitanda, alikutana na gazeti la udaku ambalo Anifa alikuwa akilisoma. Ndani yake kulikuwa na picha ya mwanamke mmoja maarufu mjini akiwa amepewa gari jipya, na Anifa alikuwa amezungushia picha ile duara kwa kalamu nyekundu.

Hassan alijua sasa, adui yake si umaskini, bali ni tamaa iliyoingizwa na watu wa nje.

---
**Je, Anifa atakubali kwenda kwenye ile pati ya usiku? Na Hassan atafanya nini akigundua mke wake anataka "kutoka nje ya mstari"? Usikose Sehemu ya 4.**