✦ Matangazo ✦

📖 Story Tamu

Episode 6: Ushauri wa X-Ray na Hospitali ya Kwanza

Ilikuwa ni siku ya Alhamisi asubuhi. Juma alikuwa amekaa sebuleni ameshika kichwa, huku akitazama kikombe cha chai ambacho kilikuwa kimepoza bila kuguswa. Usingizi haukumshika usiku kucha baada ya kumsikia mkewe akililia bafuni. Neema alitoka bafuni akiwa anashtatuka kwa maumivu, mkono wake mmoja ukiwa umeshika kiuno na mwingine ukishikilia tumbo la chini. Safari hii, maumivu yalikuwa yamebadilika; yalikuwa yakichoma kuanzia chini ya kitovu, yanapanda kwenye nyonga na kusambaa hadi kwenye pingili za mgongo.

"Mke wangu, basi imetosha," Juma alisema kwa sauti ya upole lakini iliyovunjika nguvu. "Leo ni Alhamisi. Hali hii siyo ya kawaida kabisa. Unazidi kuisha, na sasa hivi hata kutembea unashindwa kwa sababu ya mgongo na kiuno. Lazima twende hospitali leo."

Neema alijilaza kwenye kochi kwa unyonge, akijaribu kuvuta pumzi ndefu. Alimtazama mumewe kwa macho yaliyojaa dharura. "Mume wangu... naomba uende kwanza kazini leo asubuhi, kuna mambo ya maana unatakiwa kukamilisha. Mimi nitaenda kazini kwangu nikazuge kidogo, niombe ruhusa rasmi kwa bosi wangu. Alafu kesho Ijumaa asubuhi, unapoenda kazini unishushe kabisa hospitali kubwa hapa Kahama tukafanye vipimo. Nilikuwa nachukulia kawaida tu, nahisi ni gesi."

Juma alitazama saa ya ukutani, akavuta pumzi na kukubali kwa shingo upande. "Sawa mke wangu, lakini hakikisha unaomba hiyo ruhusa. Kesho asubuhi hakuna visingizio, nakupeleka mimi mwenyewe."

Mchana wa siku hiyo, mimi Salome nilifika pale ofisini kwa Neema baada ya kukosa amani tangu nilivyomwona jana yake. Nilimkuta amekaa kwenye kiti cha ofisi, lakini alikuwa ameweka mto nyuma ya mgongo wake, uso wake ukiwa umekunjana kwa maumivu makali ya pingili za kiuno.

"Dada Neema, mbona bado unateseka hivi na unalazimisha kukaa kazini?" Nilimfokea kwa upendo huku nikimshika mabega. "Haya maumivu ya kiuno na tumbo yanakwenda mbali sasa. Mimi nakushauri kesho ukienda hospitali, usikubali kupewa tu madawa ya kawaida. Waambie wakupige X-ray ya mgongo na nyonga, na wakufanyie Ultrasound kubwa ya tumbo ili waone ndani kuna nini. Humu ndani kuna kitu hakiko sawa."

Neema alinishika mkono, mkono wake ulikuwa wa baridi sana. "Sawa mdogo wangu Salome... shemeji yako ameshasema kesho asubuhi ananipeleka. Nitafanya hivyo vipimo."

Siku ya Ijumaa asubuhi ikawadia. Juma alitimiza ahadi yake; alimbeba Neema kwenye gari lake akampeleka hadi kwenye moja ya hospitali teule na kubwa hapo Kahama. Mimi nilikuwa tayari nimeshafika pale kuwasubiri. Neema alikuwa hawezi hata kutembea vizuri, alikuwa akishikiliwa pande zote mbili—mimi upande mmoja na Juma upande mwingine.

Daktari aliyekuwa zamu alimsikiliza Neema kwa makini. Neema alielezea maumivu ya tumbo, kuharisha, na jinsi kiuno na mgongo vinavyomkata, lakini bado alichagua kuificha siri ya kile kopo la vidonge na unga wa kahawia alivyokuwa anavitumia kwa siri nyumbani. Daktari aliandika karatasi ya vipimo vya haraka.

Mchakato ulianza. Neema alipelekwa chumba cha X-ray kwa ajili ya kuangalia pingili za mgongo na mifupa ya nyonga, kisha akapelekwa chumba cha Ultrasound ambapo daktari alipaka jeli ya baridi kwenye tumbo lake lililosinyaa na kuanza kuzungusha kifaa cha kuangalia viungo vya ndani kwenye kioo cha kompyuta.

Baada ya saa mbili za kusubiri kwa hofu kubwa, majibu yalivunjwa na daktari akatuita chumbani kwake.

"Haya, mmewe na mdogo wake, karibuni mkae," daktari alisema huku akitazama picha za X-ray na makaratasi ya majibu. "Kwenye picha ya X-ray, pingili zote za mgongo ziko sawa kabisa, wala mifupa ya nyonga haina shida yoyote ile. Na kwenye Ultrasound tuliyoipiga, maeneo yote yanaonekana yapo safi, hakuna shida yoyote kubwa."

Juma alishusha pumzi ndefu kwa nafuu, akizani janga limeisha. "Basi daktari, shida ni nini mbona anaharisha sana na kukonda?"

"Inaonekana ni shida ya amiba au gesi tu ya kawaida iliyochafua mfumo wa chakula," daktari alijibu kwa urahisi. Alichukua kalamu na kuandika cheti cha dawa. "Nimemwandikia dawa kali za kutuliza maumivu (painkillers) na dawa za kuzuia gesi na kurekebisha utumbo. Atumie hizi, atakuwa sawa kabisa."

Walirudi nyumbani huku Neema akiwa ameshikilia mfuko wa dawa. Lakini mimi moyoni mwangu, nilihisi kuna kitu kimejificha. Dawa zile zilitakiwa kuwa suluhisho, lakini hazikujua kuwa zilikuwa zinakwenda kukutana na utumbo uliokuwa umesababishiwa majeraha ya ndani kwa ndani na kemikali hatari za yale madawa ya siri.

---

**Katika Episode Inayofuata (SURA YA 7: Rangi ya Kahawia na Kupungua kwa Kasi):**
Dawa za hospitali zinalemaza tu maumivu kwa masaa machache, lakini baada ya hapo, hali ya Neema inalipuka na kuwa mbaya zaidi. Anaanza kuharisha kitu cha rangi ya kahawia ya kutisha na anakataa kula kabisa hadi kulazimishwa. Mimi Salome nitatoa wazo gani mbadala tunapoona hospitali ya kwanza imeshindwa? Usikose kufuatilia Sura ya 7!