✦ Matangazo ✦

πŸ“– Story Tamu

Episode 4: Kivuli cha Saraphina

Nilibaki nimekodoa macho, uma uliokuwa mkononi ulinidondoka na kugonga sahani. Kelele ile ya "ting'" ilinirudisha kwenye uhalisia. Nilimtazama Samβ€”kijana mtanashati aliyenilipia chakula njiani, aliyenibebea begi, na aliyenitafutia hifadhi usikuβ€”kumbe ndiye bosi wa kampuni kubwa niliyokuwa nikiipigia magoti nipate kazi!

"Sam... yaani wewe ndiye mkurugenzi?" nilisema kwa sauti ya chini, nikiwa nimejaa aibu isiyo na kifani. "Kwanini hukuniambia tangu mwanzo? Nimekuambia siri zangu zote, nimekulilia, nimekuelezea hadi shida za kaka yangu... naona aibu sana!"

Sam alicheka kwa sauti ya chini, akasogeza kiti chake karibu na mimi na kunishika mkono. "Tedy, usione aibu. Nilichotaka ni kumjua Tedy halisi, siyo Tedy anayeomba kazi. Na nimejua kuwa wewe ni mwanamke mwenye msimamo, mpambanaji, na mwenye akili. Interview uliyoifanya leo, uliifanya mbele ya wasaidizi wangu, na wote wamenitumia ripoti kuwa ulikuwa bora kuliko wote."

Nilihisi uso unanipata moto. Nilishusha pumzi ndefu kujaribu kutulia. "Kwahiyo... nimepata kazi?"

Sam alitabasamu na kunikonyeza. "Kazi ni yako Tedy, lakini kwa sharti moja. Usiniite 'Boss' tukiwa nje ya ofisi. Mimi bado ni yule Sam wa kwenye basi la Shabiby."

Tulimaliza kula na kuanza safari ya kurudi Dar es Salaam kwa ndege, safari ambayo kwangu ilikuwa ni ya kwanza maishani. Tulifika Dar jioni na Sam alinipeleka kwenye nyumba moja nzuri maeneo ya Upanga. Aliniambia kuwa hiyo ni nyumba ya kampuni na nitakaa hapo kwa muda mpaka nitakapopata utaratibu wangu.

Siku iliyofuata, ilikuwa ni siku yangu ya kwanza kuripoti kazini. Nilivaa vazi langu la kujiheshimu, nikajipodoa kidogo na kuelekea ofisini. Mapokezi nilipokelewa kwa heshima zote. Nilielekezwa ofisi yangu ambayo ilikuwa jirani kabisa na ofisi ya Mkurugenzi Mkuuβ€”Sam.

Nikiwa bado najiweka sawa kwenye kiti changu kipya, mlango ulifunguka kwa kishindo. Alikuwa ni mwanamke mmoja mrembo sana, aliyevaa nguo za gharama na kupaka wanja mzito. Alinitazama kwa dharau tangu miguuni hadi kichwani.

"Wewe ndiye yule binti mpya aliyekuja na Sam jana?" aliniuliza kwa sauti ya ukali na kiburi.

"Ndio, naitwa Tedy. Samahani, wewe ni nani?" nilimjibu kwa adabu.

"Mimi naitwa **Saraphina**. Na kuanzia leo, elewa jambo moja; Sam ni mchumba wangu, na hivi karibuni tutafunga ndoa. Usijaribu kuvuka mipaka yako ya kikazi, la sivyo utajikuta unarudi kijijini kwenu Songea kabla mshahara wa kwanza haujatoka!"

Aligeuka na kuondoka huku akigonga viatu vyake kwa madaha. Nilibaki nimepigwa na butwaa. Moyo ulianza kunidunda kwa nguvu. Kumbe Sam ana mchumba? Na ni mwanamke mwenye roho ya namna hii?

Wakati bado natafakari, Sam aliingia ofisini kwangu akiwa na tabasamu. "Vipi Tedy, umeanza kuzoea mazingira?"

Nilimtazama Sam kwa macho yaliyojaa maswali. "Sam... Saraphina ni nani?"

Tabasamu la Sam lilipotea ghafla. Alivuta kiti na kuketi mbele yangu. "Tedy, nisikilize vizuri. Kuna mambo mengi unayopaswa kuyajua kuhusu Saraphina na mimi, na siyo kila unachokiona ni ukweli."

---
**Inaendelea Sehemu ya 5...**