✦ Matangazo ✦

πŸ“– Story Tamu

Episode 2: Malaika wa Giza

Baada ya kunishusha taratibu kwenye zile ngazi za basi, Sam hakuniacha mkono mapema. Alinitazama machoni kwa sekunde kadhaa ambazo zilinitoa kwenye mstari. Moyo ulinienda mbio, nikajihisi kama nimefika sehemu salama ambayo sikutakiwa kuondoka.

β€œUko sawa Tedy? Usije ukateleza, hizi ngazi zina ujanja wake,” aliniambia huku akinitabasamu lile tabasamu lake la gharama.

Niliitikia kwa kichwa tu, maneno yalikwama kooni. Nilienda msalani na niliporudi, nilimkuta amenisubiri pembeni ya mlango wa basi. Tulipanda na safari ikaendelea kuelekea Dodoma. Tukiwa njiani, mazungumzo yetu yalizidi kunoga. Sam alikuwa mcheshi, mwenye busara, na alijua kupangilia maneno kiasi kwamba muda ulikimbia bila mimi kujua.

β€œTedy, ukifika Dodoma una mwenyeji? Au ndio unakwenda kuanza maisha mapya kabisa?” aliniuliza huku akinitazama kwa makini.

Swali hilo lilinirudisha kwenye uhalisia wa maisha yangu. Nilikumbuka jinsi kaka yangu alivyofungia kila kitu, na jinsi sikuwa na uhakika wa wapi nitalala usiku huo. Nilikuwa na namba ya simu ya rafiki yangu mmoja wa chuo, lakini hakuwa amepokea simu yangu tangu asubuhi.

β€œNina rafiki yangu huko, naamini nitafika salama,” nilijibu kwa sauti ya kusuasua, nikijaribu kuficha wasiwasi wangu.

Sam alihisi kitu. β€œKama utapata changamoto yoyote, usisite kuniambia. Mimi ninafanyia kazi kampuni moja kubwa ya utalii hapa Dodoma, na nitakuwepo kwa siku kadhaa kabla ya kurudi Dar.”

Giza lilianza kuingia na taa za barabarani za jiji la Dodoma zikaanza kuonekana kwa mbali. Tulifika stendi ya Nanenane (Nzuguni). Watu walianza kushuka. Moyo ulinidunda kwa nguvu; hapa ndipo safari ya Sam na Tedy ilikuwa inafika kikomo. Nilijisikia mpweke ghafla kabla hata sijaondoka kwenye kiti changu.

Tulishuka wote. Sam alibeba begi lake dogo la mgongoni. Alisimama mbele yangu na kutoa kadi yake ya kazi (business card).

β€œTedy, hii ni namba yangu. Hakikisha unanijulisha kama umefika salama kwa rafiki yako. Na pia, nikutakie kila la heri kwenye interview yako ya kesho. Naamini utapasua!”

Nilipokea ile kadi kwa mikono inayotetema. Tulipeana mkono wa kwaheri, lakini yeye aliniivuta kidogo na kunikumbatia kukumbatia kwa haraka. Harufu ya pafyum yake ilibaki kwenye nguo zangu. Alipanda taksi na kuondoka, nikaingia kwenye upweke wa jiji la kigeni.

Niliipiga namba ya rafiki yangu... haikupatikana. Nilipiga tena na tena, wapi! Giza lilizidi na baridi ya Dodoma ikaanza kunikata. Niliketi kwenye benchi moja stendi pale, machozi yalianza kunilenga. Sikuwa na hata shilingi mia tano ya kulipia gesti ya bei rahisi, na sikutaka kumsumbua mgeni (Sam) niliyemjua safarini.

Saa nne usiku, nikiwa nimekata tamaa na begi langu mkononi, simu yangu iliita. Nilitumaini ni rafiki yangu, lakini jina lililoonekana lilikuwa ni namba ngeni. Niliipokea.

β€œHalo Tedy, ni mimi Sam. Umeshafika kwa rafiki yako? Mbona moyo wangu umekataa kutulia tangu nimekuacha pale stendi?”

Sikuweza kujizuia. Nilianza kulia kwa kwikwi kwenye simu.

β€œSam... rafiki yangu hapatikani, na mimi hapa stendi sielewi pa kwenda...” nilisema huku nikilia.

β€œUsiondoke hapo! Nakaa kwenye taksi sasa hivi nakuja kukuchukua. Tulia hapo hapo Tedy, nakuja.”

Baada ya dakika kumi na tano, gari ilisimama mbele yangu. Sam alishuka akiwa na wasiwasi mwingi. Alinikumbatia kwa nguvu huku akinituliza. Alinipeleka kwenye hoteli moja ya kifahari ambapo yeye alikuwa amefikia. Aliniombea chumba kingine pembeni ya chumba chake.

β€œPumzika hapa Tedy. Kesho asubuhi tutaongea, na nitakufikisha kwenye interview yako mwenyewe. Usiwe na wasiwasi, mimi nipo hapa kwa ajili yako sasa.”

Nilijitupa kitandani, nikitazama dari ya chumba kile cha kifahari. Nilijiuliza, huyu kaka ni malaika au ana malengo gani na mimi? Na je, interview ya kesho itakuwaje?

---
**Inaendelea Sehemu ya 3...**