✦ Matangazo ✦

📖 Story Tamu

Episode 1: Safari ya Matumaini

“Dada naona unaumia shingo, unaweza lala kwenye bega langu ili upate kupunguza maumivu ya shingo yako,” sauti ya kaka aliyeketi pembeni yangu ndani ya gari iliniambia kwa utaratibu na sauti yenye kujiamini.

Nilitabasamu kidogo na kumshukuru. Ni kweli nilikuwa naumia shingo. Taratibu nilijilaza kwenye bega lake; bega lilikuwa na nyama nyingi hivyo sikulalia mifupa. Nyimbo ya taratibu iliyokuwa inapiga ndani ya gari ilinifanya nipate usingizi mwanana.

Huo ulikuwa msaada wa pili kutoka kwa kaka huyo. Msaada wa kwanza ulikuwa ni wa kuniachia siti ya dirishani. Safari ya kuelekea Dodoma ilikuwa katika uzuri wake kwani dereva hakuendesha kwa mwendokasi sana wala taratibu sana, yaani ilikuwa wastani. Nilikuwa ndani ya basi la **Shabiby Line** lenye kiyoyozi cha kutosha.

Tulipofika Morogoro mjini, gari iliingia kwenye hoteli moja kwa ajili ya mapumziko na chakula. Kaka wa pembeni aliniamsha kwa sauti yake ile ile yenye utulivu mwingi na ustaarabu usiohesabika.

“Tupo hotelini neighbor, vipi unashuka?”

Nilimjibu hapana. Sikutaka kushuka kwenye hoteli hiyo kwani nilijua vyakula vya mahoteli mengi ya njiani ni ghali sana, na mimi sikuwa na pesa mfukoni kabisa. Ilikuwa safari ya kavu kavu. Muhimu kwangu ilikuwa nifike Dodoma ili niende kwenye usaili (interview). Hiyo ilikuwa interview ya muhimu sana kwenye maisha yangu; ilikuwa nafasi ambayo sikutaka kuipoteza kabisa kwani bila kupita hapo, nilikuwa naharibu maisha yangu kabisa.

Kabla ya kuanza safari, kaka yangu aliniambia nisirudi nyumbani kwake tena baada ya kuingia kwenye ugomvi na mkewe (wifi yangu). Nilipaswa kurudi kijijini kwetu huko Songea. Majibu yalipotoka kuwa interview inafanyika Dodoma, ndipo kaka aliniuliza anikatie tiketi ya kwenda Songea au ya Dodoma. Nilichagua Dodoma kujaribu bahati yangu. Alidai tiketi hiyo ndio msaada wake wa mwisho, lakini akanikatia basi la gharama (Luxury) na hakunipa pesa ya matumizi njiani hata senti moja. Alinijibu kama nataka nipande, nikaondoka bila namna nyingine.

Kaka jirani aliomba apite, nilimpisha akashuka. Baada ya dakika kama sita, alirudi akiwa na vimfuko viwili. Alinipatia kimoja na kuniambia:

“Hii ni kwa ajili yako, ni safi na salama, usikatae please.”

Sikuwa na kawaida ya kula chochote nilichopewa na mgeni nisiemjua kwa tahadhari ya usalama, ila kwa maneno ya huyu kaka, nilishindwa kukataa. Nilijikuta napokea na kumshukuru. Nilipofungua ule mfuko, kulikuwa na **soda ya kopo** (Pepsi ya baridi sana) na **chips kuku** zenye soseji mbili. Mate yalinitoka haswa kwani chakula kilikuwa kinanukia vizuri sana.

Nilitabasamu na kuanza kula taratibu. Huo ndio ulikuwa muda ambao nilianza kumjua. Kaka neighbor anaitwa **Samson**, japo aliniambia anapenda kuitwa **Sam**. Na mimi nikajitambulisha kuwa naitwa **Theresia**, lakini aniite **Tedy**.

Tulimaliza kula na mazungumzo ya kawaida yalianza. Aliniuliza kama nafika Dodoma mjini au nashukia njiani. Nilimjibu naenda mpaka Dodoma mjini kwenye interview ya kazi. Alinipongeza sana na kuanza kunipa mbinu za kufanya vizuri kwenye usaili.

Huo uongeaji wake, macho yake mazuri, na jinsi alivyokuwa ananitazama ilikuwa ni "hatari" mwanzo mwisho. Kingine kilichonivutia ni jinsi alivyokuwa amenukia vizuri; alikuwa na harufu ya pafyum kali ambayo sikutambua jina lake. Alivaa tishati ya kijivu na suruali ya kitambaa iliyomkaa vizuri mwilini mwake.

Tulipokuwa tunaendelea na safari, pembeni yetu kulikuwa na mdada aliyekuwa anatapika sana. Sam alifungua kibegi chake kidogo, akatoa dawa na kumpatia yule dada. Baada ya muda, yule dada alipona na kumshukuru sana Sam. Hapo ndipo niliona Sam ana moyo wa huruma sana kwa watu.

Gari liliingia kwenye hoteli nyingine, aliniuliza kama nashuka, nikamwambia ndio kwa ajili ya kwenda chooni. Tulipofika kwenye ngazi za kushuka basi, aliniomba mkono ili anishushe taratibu asije kuniumiza. Aliniangalia kwa makini sana wakati ananishusha...

---
**Inaendelea Sehemu ya 2...**