✦ Matangazo ✦

📖 Story Tamu

Episode 13: Machafuko ya Peramiho

Usiku ule wa kwanza kijijini Peramiho ulikuwa na baridi kali ya asili, lakini baridi niliyokuwa naisikia mimi ilikuwa ya tofauti. Tulikuwa tumetenga vitanda; mimi nililala chumba cha ndani na wazazi, na Sam alipewa chumba cha wageni kilichokuwa kimeandaliwa vizuri na kaka yangu.

"Tedy... Tedy... njoo huku..."

Sauti hiyo ilikuwa ya chini, kama upepo unavyovuma kwenye majani ya migomba. Niliamka na kukaa kitandani, moyo ukinidunda. Nilitazama dirishani, giza lilikuwa nene lakini nikaona kivuli cha mtu kimesimama nje. Nilihisi hofu kubwa, nikakumbuka onyo la mama kuwa kijijini hapo watu wana husuda sana na mafanikio ya wengine.

"Nani huyo?" niliuliza kwa sauti ya kutetemeka.

Kivuli kile kilitoweka ghafla. Nilitoka kitandani na kwenda chumba cha Sam kuona kama yuko salama. Nilimkuta amelala fofofo, uso wake ukiwa na amani. Nilikaa pembeni yake na kuanza kulia kwa sauti ya chini. "Boss, naona aibu! Nimekuleta kijijini kwetu ili upate baraka, kumbe nimekuleta kwenye hatari?"

Asubuhi ilipofika, tuliamka na kuanza maandalizi ya kutoa posa rasmi. Sam alikuwa amejipanga; alileta suti mbili kwa ajili ya baba yangu na vitenge vya gharama kwa ajili ya mama. Pia alikuwa na bahasha nene ya mahari ambayo wazazi wangu hawajawahi kuiona maishani mwao.

Wakati wa mazungumzo, Vick alikuja tena nyumbani akiwa amebeba ndoo ya maji, akijifanya anapita kuelekea kisimani. Alisimama na kumkodolea Sam macho. Sam, kwa ukarimu wake wa kawaida, alitoa noti mbili za elfu kumi kumi na kumkabidhi Vick.

"Chukua hii ukawanunulie watoto matunda," Sam alisema kwa tabasamu.

Vick alipokea zile pesa kwa mikono miwili huku akipiga magoti, lakini kicheko chake cha chini kiliniashiria kuwa hakuwa na shukrani. Aliondoka haraka. Mara baada ya Vick kuondoka, nikaanza kuhisi kizunguzungu kikali. Macho yangu yalianza kuona malue-lue; niliona kama nyumba inageuka na watu wanakuwa na vichwa vya wanyama.

"Tedy! Una nini mwanangu?" Mama alipiga kelele baada ya kuniona naanza kuweweseka na kukimbia hovyo uwanjani.

Nilianza kutaja majina ya ndugu zangu waliokufa miaka mingi iliyopita. Nilianza kuvua nguo zangu mbele ya watu, nikicheka na kulia kwa wakati mmoja. Sam alishtuka na kunikamata kwa nguvu, lakini nilikuwa na nguvu za ajabu; nilimshindilia chini na kuanza kumkaba koo huku nikisema kwa sauti ya kiume: "Huyu binti hamumpi huyo mgeni! Huyu ni wa hapa hapa kijijini!"

Kaka yangu aliyekuwa anajua mambo ya kijijini, alikimbia haraka hadi kijiji jirani cha Mpitimbi kumfuata bibi mmoja mtaalamu wa manyanga. Wakati huo, Sam alikuwa amelia machozi akiona mchumba wake amechanganyikiwa ghafla.

Bibi mganga alipofika, alitazama kiganja changu na kisha akachukua chungu chake cha maji. Alitupa punje za mahindi ndani ya chungu na kutuambia sote tuchungulie. Kwenye yale maji, tulimwona Vick akiwa ameshika mchanga wa nyayo zangu na zile pesa alizopewa na Sam, akizichoma moto mbele ya mti mkubwa wa mbuyu huku akitaja jina langu.

"Husuda ni mbaya kuliko sumu ya nyoka," Bibi mganga alisema huku akianza kupiga manyanga yake. "Vick alitaka Tedy abaki hapa kijijini awe mwendawazimu ili asiolewe na huyu bosi, kwa sababu yeye (Vick) ana maisha magumu na watoto wanne bila mume."

Bibi mganga alianza kufanya mambo yake. Alichukua ule ugonjwa na kuufunga kwenye kitambaa cheusi. "Sasa, huu ugonjwa nanamrudishia mwenyewe aliyewatuma!"

Ghafla, nilizinduka na kuwa mzima. Nilikuta nimefungwa kamba mikononi na miguuni. Nilimwona Sam akiwa amelowa jasho na machozi akinitazama. Lakini kabla hatujasema neno, tulisikia kelele za kutisha kutoka nyumba ya jirani... ilikuwa ni sauti ya Vick akipiga yowe na kuanza kukimbia uchi kuelekea sokoni!

---
**Inaendelea Sehemu ya 14...**