📖 Story Tamu

Episode 5: DHAMBI YA MWISHO

Hali ilikuwa ya kutisha. Juma alikuwa akimsogelea Neema huku kisu mkononi kikimetameta kwa mwanga hafifu wa kile kijani kibichi kinachotokea chumba cha siri. Neema alikuwa akijivuta kwa nyuma akilia kwa sauti ya kukata tamaa, huku mimi nikitafuta upenyo wa kumzuia rafiki yangu asitumbukie kwenye shimo la damu.

"Juma! Kumbuka tulipotoka! Kumbuka mama yako kule kijijini anavyokusubiri kwa heshima! Ukimwaga damu hii, hutakuwa na amani milele!" nilipiga kelele nikijaribu kumrudisha kwenye akili ya kibinadamu.

Juma alisimama kwa sekunde chache. Mkono wake uliokuwa umeshika kisu ulianza kutetemeka. Macho yake yalianza kutoa machozi ya kawaida, yakichanganyika na ile rangi ya njano. "Mwanangu... siwezi kurudi kwenye umaskini. Siwezi kuwa yule dereva wa Taxi anayesimangwa kila siku. Siwezi!"

Ghafla, lile kivuli kirefu kilichokuwa nyuma yake kilimshika mabega. Juma alipiga yowe kama amechomwa na pasi ya moto, na hapo hapo hofu yote ikatoweka usoni mwake. Akabaki na uso wa kikatili. Alimrukia Neema!

"Hapana!" nilipiga kelele na kumrukia Juma kwa nyuma. Tuligubikana sakafuni, tukipigana mieleka. Juma alikuwa na nguvu za ajabu, kana kwamba anasukumwa na injini. Alinitupa pembeni kama gunia la pumba, nikagonga kabati la kioo ambalo lilipasuka na kunichana begani.

Juma alimfikia Neema na kumkamata nywele zake. Alimvuta kuelekea kile chumba cha siri. Neema alikuwa akipiga kucha sakafuni akijaribu kujishika, lakini sakafu ilikuwa imekuwa telezi kama kuna mafuta yamemwagika.

"Niingize! Niingize nimtoe kafara!" Juma alikuwa akiongea na viumbe vile visivyoonekana.

Lakini alipofika tu mlangoni mwa kile chumba cha siri akiwa amemvuta Neema nusu mwili, kitu cha ajabu kilitokea. Kile kiumbe kilichomo ndani ya tumbo la Neema kilionekana kucheza kwa nguvu. Neema alipiga ukelele mkali wa maumivu, na ghafla mwanga mweupe na mkali sana ulilipuka kutoka mwilini mwa Neema.

Ule mwanga ulikuwa na nguvu ya ajabu. Vile vivuli vilivyokuwa nyuma ya Juma vilipiga kelele za kuungua na kutokomea ndani ya kile chumba. Juma naye alirushwa mbali na ule mwanga, akagonga ukuta na kuanguka chini akiwa hajitambui.

Kile chumba cha siri kilianza kutoa sauti ya mlipuko. Moto wa ajabu, moto wa bluu, ulianza kuwaka ndani ya chumba kile.

"Neema! Amka! Toka hapo!" nilimkimbilia Neema na kumvuta kwa nguvu kuelekea mlangoni.

Ile kufuli ya kishirikina iliyokuwa mlangoni iliyeyuka kama nta. Nilifanikiwa kuufungua mlango mkuu. Nilimbeba Neema mkononi mmoja na kumvuta Juma kwa mkono mwingine, tukatoka nje ya lile jumba.

Tulipofika uwanjani, tuligeuka kutazama. Lile hekalu la Juma lilikuwa likimezwa na ardhi polepole. Kila gari, kila pikipiki, na kila kitu cha thamani kilikuwa kikigeuka kuwa majivu na mchanga mbele ya macho yetu.

Simu ya Juma iliyokuwa mfukoni mwake ilitoa sauti ya meseji ya mwisho:
> *"Umechelewa. Masharti hayajavunjwa na mwanamke, yamevunjwa na hofu yako. Sasa, kila kitu kimerudi kule kilipotoka."*

Juma alizinduka na kuanza kulia kwa sauti ya kukwaruza. Alitazama mikono yake; ile pete ya dhahabu ilikuwa imegeuka kuwa kipande cha mfupa wa mnyama. Alitazama uwanja wake; hakukuwa na Fuso, hakukuwa na kuta za ghorofa. Palikuwa na pori na magofu ya zamani.

"Nimepoteza kila kitu... nimepoteza kila kitu!" Juma alikuwa akigaragara kwenye vumbi.

Lakini je, huu ndio ulikuwa mwisho? Au wale viumbe walikuwa bado wanadai deni lao kwa namna nyingine?

**Usikose Sehemu ya 6...**
Matangazo
Matangazo