✦ Matangazo ✦

📖 Story Tamu

Episode 17: Hakimu wa Amani

Maisha ya Mbezi Beach yalikuwa ya ndoto. Kila asubuhi nilionja ladha ya utajiri ambayo mwanafunzi yeyote wa "BIT Stream A" angeitamani. Caroline alinifanya nionekane mfalme; suti za gharama, gari la ofisi, na harufu ya manukato yaliyoziba kabisa ile harufu ya udi ya Malha. Lakini moyoni mwangu, nilihisi kama ndege aliyefungiwa kwenye tundu la dhahabu.

"Tom, mbona unawaza sana? Leo ni siku yetu kubwa," Caroline aliniambia huku akinirekebisha tai yangu mbele ya kioo kikubwa. "Nataka kila mtu ajue kuwa wewe ndiye mwanaume aliyenituliza."

"Niko sawa Caroline, ni msisimko tu wa hafla ya leo," nilidanganya kwa tabasamu langu la kizoefu.

Tulifika kwenye ukumbi wa kifahari wa hoteli ya *Serena*. Taa zilikuwa ziking'aa, na viongozi mbalimbali wa kibiashara walikuwa wakimshika mkono Caroline kwa heshima. Nilikuwa pembeni yake kama pambo la thamani. Lakini katikati ya vicheko na glasi za mvinyo, macho yangu yalitua kwenye mlango wa kuingilia.

Binti mmoja alikuwa amesimama pale, amevaa gauni refu la rangi ya kijani kibichi, uso wake ukiwa umefichwa kiasi na kofia ya kike. Alikuwa ni **Lisa**! Hakuwa anaonekana kama yule binti mnyonge wa stendi ya Tanga; alikuwa amependaza na alikuwa na ujasiri usio wa kawaida. Pembeni yake alikuwa mwanaume mmoja mwenye umri wa makamo, aliyeonekana kuwa na mamlaka makubwa.

"Caroline, mgeni wetu wa heshima amefika," mratibu wa hafla alitangaza. "Mkaribishe **Mzee Jumanne**, hakimu mkuu mstaafu na mwekezaji wetu mpya."

Caroline alitabasamu na kusogea kuwakalibisha. Lakini alipomuona Lisa pembeni ya Mzee Jumanne, uso wake ulibadilika rangi. "Lisa? Wewe unafanya nini hapa na Mzee Jumanne?"

"Huyu ni mjukuu wangu, Caroline," Mzee Jumanne alisema kwa sauti nzito yenye mamlaka. "Alinitafuta kule Tabora na kuniambia madhila yote aliyopitia hapa Dar es Salaam. Akaniambia kuhusu kijana mmoja anayeitwa Tom na kiapo chao cha damu ambacho kimekuwa kikitumiwa kama fimbo ya kumnyanyasa."

Ukumbi mzima ukawa kimya. Macho yote yakatugeukia mimi na Caroline. Lisa alinipitisha macho kama hanijui, kisha akamtazama Caroline kwa dharau.

"Caroline, ulidhani pesa zako zinaweza kununua kila kitu?" Lisa alianza kuongea, sauti yake ikitetemeka kwa hasira iliyofichwa. "Ulimlipa dereva wako anipeleke Tabora, lakini ulijua fika kuwa mjomba wangu ni nani? Mimi nimerudi 'kuchukua changu', na changu siyo pesa zako, bali ni utu wangu na haki yangu kwa Tom."

Mzee Jumanne alikohoa kidogo. "Leo siko hapa kibiashara pekee. Nimekuja kama 'Hakimu wa Amani'. Tom, nimeambiwa wewe ni mwanafunzi mwenye akili lakini umepoteza mwelekeo. Je, unataka kuendelea kuwa 'mzoefu' wa kuchezewa na wanawake wenye pesa, au unataka kutimiza kiapo chako kwa binti huyu aliye tayari kufa kwa ajili yako?"

Caroline aliniandama mkono kwa nguvu, kucha zake zikinitoa maumivu. "Tom, usithubutu. Kumbuka nimefanya nini kwa ajili yako. Kumbuka kile chumba chako cha uswahilini na njaa uliyokuwa nayo."

Nilihisi kama niko kizimbani. Upande mmoja ni Caroline, aliyeniokoa mikononi mwa Robby na Malha na kunipa maisha ya kifahari. Upande wa pili ni Lisa, mpenzi wangu wa asili ambaye sasa ana mgongo wa mamlaka ya Mzee Jumanne.

Ghafla, simu yangu ilitetemeka mfukoni. Ulikuwa ujumbe wa picha kutoka kwa namba ya **Dora**, aliyekuwa amebaki nyumbani kwa Caroline. Picha hiyo ilionyesha nyaraka fulani ambazo Caroline alikuwa amezificha kwenye droo yake ya siri.

*"Tom, kimbia! Caroline ameshaanza mchakato wa kukuhamishia deni la milioni hamsini la Robby kwa jina lako! Ukisaini mkataba wa mkurugenzi usiku wa leo, utakuwa mfungwa wa madeni yake maisha yako yote!"*

Nilitazama ule mkataba uliokuwa mezani ukisubiri saini yangu kama "Mkurugenzi wa Masoko." Mwamvuli wa Caroline sasa ulikuwa unageuka kuwa mtego wa chuma.

Nilimtazama Mzee Jumanne, kisha nikamtazama Lisa. Nilivuta pumzi ndefu na kuuachia mkono wa Caroline.

"Mzee Jumanne, niko tayari kusema ukweli," nilisema kwa sauti iliyosikika kumbi nzima. "Mimi si mzoefu wa mapenzi, mimi ni mzoefu wa makosa. Na leo, nataka kuanza upya."

Lakini kabla sijamaliza, taa za ukumbi zilizima ghafla. Sauti ya kishindo ikasikika, na mtu mmoja akapiga yowe. Taa zilipowaka tena, Lisa alikuwa ameshatoweka, na mahali alipokuwa amesimama, palikuwa na **mwamvuli mwekundu** uliokuwa na alama ya udi... alama ya Malha!

**ITAENDELEA SEHEMU YA 18...**