✦ Matangazo ✦

📖 Story Tamu

Episode 10: Usiku wa Usaliti

Harufu ya udi chumbani kwa Malha ilikuwa ikinizidisha ulevi wa mahaba, lakini ujumbe wa Caroline ulikuwa kama msumari wa moto uliopigwa kichwani mwangu. "Niko mlangoni kwako!" Maneno yale yalinifanya nitokwe na jasho la baridi kifuani. Caroline alikuwa amebeba funguo za maisha yangu ya baadaye—kazi, pesa, na heshima mjini. Lakini Malha? Malha alikuwa amebeba funguo za moyo wangu na utamu ambao sikuwahi kuuonja.

"Mpenzi, mbona umekuwa kama kigutu? Kuna nini kwenye hiyo simu?" Malha aliniuliza kwa sauti ya kulevya, huku akipitisha vidole vyake laini kwenye mgongo wangu.

"Ah... hapana Malha. Ni mwalimu wangu wa shule, anasema kuna mabadiliko ya ratiba ya mtihani wa kesho asubuhi," nilidanganya kwa ujasiri wa hali ya juu, uzoefu wangu wa kusema uongo ukiwa sasa umefikia kiwango cha 'PhD'.

"Basi usijali, mimi nitakuamsha saa kumi na moja ili uwahi. Lakini sasa hivi, mimi ndiye mwalimu wako," Malha alinong'ona na kunivuta tena kitandani.

Moyo ulinidunda. Caroline alikuwa nje ya mlango wangu wa kupanga, akisubiri kwa upendo na zawadi, huku mimi nikiwa nimezama kwenye bahari ya Tanga. Niliamua kufanya kitu cha hatari. Niliiandika namba ya Caroline na kumtumia ujumbe wa haraka:
*"Caroline mpenzi, nisamehe sana! Nimepata dharura, nimeitwa Tabora ghafla usiku huu, mama anaumwa sana. Nimeshaondoka na basi la usiku. Usinisubiri mlangoni, nitarudi baada ya siku mbili. Nakupenda!"*

Niliutuma ujumbe ule na kuizima simu jumla. Nilihisi kama nimeepuka bomu, lakini sikujua kuwa Caroline hakuwa mwanamke wa kudanganywa kirahisi hivyo.

Usiku ule Malha alinionyesha kwanini Tanga inaitwa "nyumbani." Alinitunza kwa staili ambazo niliziona kwenye hadithi za kusadikika tu. Kila sekunde ilikuwa na thamani ya saa moja. Nilisahau matatizo yote ya Lisa, Robby, na hata Caroline. Nilijiona mwanaume kamili.

Majira ya saa kumi na moja alfajiri, Malha aliniamsha kama alivyoahidi. Aliniandalia maji ya uvuguvugu yenye marashi, akanipikishia chai ya mdalasini na mkate wa mayai. "Nenda kapambane na shule mume wangu, nimekuombea dua utafanikiwa," aliniambia huku akinibusu paji la uso.

Niliondoka kwa Malha nikiwa na tabasamu la ushindi. Nilipofika karibu na nyumba yangu ya kupanga, niliona gari la Caroline likiwa bado limepaki pembeni ya barabara, umbali kidogo na nyumba yangu. Moyo ulinilipuka! Alikuwa hajaondoka?

Nilijaribu kujificha nyuma ya ukuta, lakini ghafla mlango wa gari ulifunguka. Caroline akatoka, akiwa amechoka na macho yake yakiwa mekundu kwa kukosa usingizi. Aliniona!

"Tom!" aliniita kwa sauti iliyojaa mshangao na hasira. "Basi la Tabora limegeuka na kukurudisha hapa saa kumi na mbili asubuhi? Na mbona nguo zako zina harufu ya udi na marashi ya kike?"

Nilistuka. Nilikumbuka harufu ya chumba cha Malha. Caroline alinisogelea, akivuta harufu ile kwa hasira. "Umenidanganya Tom. Nilikesha hapa kukulinda na kukuombea msamaha, kumbe ulikuwa unazunguka na wanawake wengine?"

Kabla sijaweza kutoa neno la utetezi, **Dora** alitoka ndani ya nyumba akiwa na kanga yake moja. "Shemeji Caroline, huyu Tom usimwamini! Jana usiku aliondoka hapa saa nne, akasema anaenda kwa nesi mmoja anaitwa Malha!"

Dunia ilizunguka. Usaliti wa Dora, hasira ya Caroline, na picha ya Malha kichwani mwangu. Hapo ndipo nilipojua, mzoefu anaweza kujua kuogelea, lakini mawimbi ya wanawake watatu kwa wakati mmoja yanaweza kumzamisha hata awe nani.

**ITAENDELEA SEHEMU YA 11...**