✦ Matangazo ✦

📖 Story Tamu

Episode 11: Namba ya Simu na Majibu ya Daktari

Maneno ya Neema yalikuwa kama dhoruba iliyoupasua moyo wangu vipande vipande. Nilibaki nimesimama huku mwili mzima ukinisisimka kwa hasira, mchanganyiko wa uchungu na mshtuko mkubwa mno. Nilimtazama dada yangu, yule aliyekuwa lango na nguzo yetu, jinsi alivyolala pale kitandani kwa unyonge, akishikilia diaper aliyovishwa huku pumzi zikimwenda kwa tabu.

"Dada... mbona ulifanya hivi?" nilisema huku nikiwa nalia kwa sauti ya chini, machozi yakinitiririka bila kuzuia. "Mbona hukuniambia mimi tangu mwanzo? Unajua jinsi tulivyohangaika Kahama, tukaenda mpaka hospitali ya kwanza wakakosa majibu, tukamleta Mchungaji, kumbe unajua chanzo ni hizo product?"

Neema alizidisha kilio, akizika uso wake kwenye ukingo wa kile kitanda cha chuma cha Bugando. "Niliogopa, Salome... niliogopa sana mume wangu akiniona mjinga. Nilitaka tu kufanya siri, liishe haraka nirejee kuwa mrembo wake..."

Alinyosha mkono wake unaotetemeka kuelekea kwenye kijipochi chake cha mkononi kilichokuwa juu ya meza ndogo ya wodini. "Chukua simu yangu... namba yake hii hapa. Nimeandika 'Aisha Product'. Nimempigia sana tangu jana, nikamueleza jinsi ninavyoharisha na kukatika utumbo, lakini yeye alisema kuwa hajawahi kusikia malalamiko ya namna hiyo kutoka kwa wateja wake, akasema labda mimi nimekosea namna ya kutumia... Salome, nisaidie kumpigia umwambie maisha yangu yanaisha."

Nilichukua ile simu kwa hasira inayofukuta moyoni. Nilifungua namba ile na kuipiga papo hapo, nikajisogeza karibu na dirisha la wodi. Simu iliita kwa muda mrefu kabla ya kupokelewa na sauti ile ile ya baridi ya mwanamke.

"Halo, nani mwenzangu?" sauti ilisikika.

"Wewe dada Aisha, naitwa Salome, mdogo wake Neema uliyemuuzia dawa za kupunguza tumbo huko Kahama!" nilifoka kwa sauti ya chini iliyojaa ukali. "Dada yangu yuko ICU hapa Bugando Mwanza! Anaharisha damu na utumbo unateketea kwa sababu ya sumu uliyomuuzia! Unajisikiaje kufanya biashara ya kuua watu?"

"Wewe dada acha kunisingizia na kuniletea mambo ya kishamba!" Aisha alifoka upande wa pili kwa ukali, sauti yake ya upole ya kibiashara ikiwa imetoweka kabisa. "Dawa zangu ni salama kabisa, zina kibali cha nje. Kama dada yako alikuwa na matatizo yake mengine ya siri msitusingizie sisi. Na usinipigie tena hii namba!" Punde si punde, alikata simu na nilipojaribu kupiga tena, alikuwa ameshaniblok.

Hasira ilinitatiza, nikajisikia upweke mkubwa dhihirisho la ukatili wa biashara hizi za mitandaoni. Nilirudi kitandani na kumkumbatia dada yangu. Nililia sana, nikamuuliza: "Dada mbona we zuri tu? Hilo tumbo la operation lingekaa sawa tu kwa kufanya mazoezi na kurekebisha chakula kama ambavyo ungekuwa na subira. Kwanini sasa uliamua kufanya hivyo na umenificha, haukunambia tangu mwanzo?"

Neema hakuwa na nguvu ya kujibu zaidi ya kulia na kunishika mkono kwa nguvu, akijuta kwa nini aliamua kuchagua njia ya mkato kumfurahisha mtu.

Ghafla, mlango wa wodi ulifunguka. Daktari bingwa aliyefanya vipimo vya *Endoscopy* na *Colonoscopy* aliingia, akifuatiwa na Juma (shemeji yangu) ambaye uso wake ulikuwa umepauka kwa hofu na mikono yake ikiwa imeshikana kwa mbele akisubiri hatomuelewa nini kitatokea.

Daktari alisimama mbele ya kitanda, akafungua lile faili kubwa. Hali ya hewa chumbani ikawa nzito mno.

"Basi, ndugu wa mgonjwa, majibu ya vipimo vya ndani vimeshatoka," daktari aliongea akitutazama sote watatu kwa zamu, macho yake yakiwa yamebeba ukweli usiofariji. "Kamera tulizozipitisha ndani ya mfumo wa chakula zimeonyesha picha ya kutisha sana. Utumbo wake wote wa chakula, kuanzia tumboni hadi utumbo mpana, una vidonda vikubwa sana vilivyochubuka na kuungua, kana kwamba amemeza kemikali kali ya kiasidi."

Juma alipiga kelele ya mshtuko, "Utumbo una vidonda na umeungua daktari? Kivipi? Mbona Kahama walisema hana shida?"

Daktari alinyosha mkono wake kumtuliza Juma, kisha akaendelea: "Hospitali ya kwanza walipiga tu Ultrasound ya nje, isingeweza kuona donda la ndani ya utumbo. Na kibaya zaidi, kuta za utumbo zimebadilika muundo kutokana na majeraha hayo ya mfululizo... Vipimo vimeonyesha wazi kuwa ana dalili kubwa za Kansa ya utumbo, na sasa hivi ipo kwenye Stage ya kwanza (Stage 1). Lazima tuchukue hatua za haraka sana kabla haijasambaa mwilini."

Maneno yale ya daktari yalizua kilio kipya na cha kutisha mle wodini. Juma alipiga magoti hapo hapo chini, akishika kichwa chake huku akishindwa kuamini dhoruba iliyomfika mkewe.

---

**Katika Episode Inayofuata (SURA YA 12: Ungamo la Machozi kwa Mume):**
Baada ya daktari kutoa majibu yale ya kansa na utumbo kuungua, Neema anashindwa kuendelea kuficha siri ile mbele ya mumewe Juma. Anaamua kufungua kinywa chake mbele ya Juma na kukiri kila kitu kuhusu ule utani uliomuumiza na kumfanya anywe zile dawa za sumu. Je, Juma atapokeaje ungamo hilo la mkewe, na nini kitafuata kitandani hapo? Usikose kufuatilia Sura ya 12!