✦ Matangazo ✦

📖 Story Tamu

Episode 10: Vipimo vya Bugando na Haki ya Siri

Mazingira ya Hospitali ya Rufaa ya Bugando yalikuwa na msisimko wa dharura za asubuhi. Madaktari bingwa na wauguzi walimzunguka Neema mara moja baada ya kumfikisha kitandani. Walimfunga mipira ya oksijeni puani ili kumsaidia kupumua, kisha wakamfanyia dharura ya kumuwekea dripu ya maji (saline) ili kufidia maji mengi aliyopoteza kwa kuharisha.

"Hali yake imeshuka sana, amepoteza maji mengi na presha yake iko chini mno," daktari mmoja mwandamizi alieleza huku akitazama mboni za macho ya Neema zilizokuwa zimefifia. "Tunapaswa kufanya vipimo vyote vikubwa vya ndani sasa hivi. Tutafanya vipimo vya damu, na kikubwa zaidi tutafanya *Endoscopy* na *Colonoscopy* ili kuingiza mipira yenye kamera maalum itakayotwambia nini kinaendelea kwenye mfumo wake wa chakula na utumbo."

Mchakato huo ulichukua masaa kadhaa ya mateso na hofu kubwa kwetu. Juma alikuwa akitembea huku na kule kwenye korido za hospitali, nguo zake zikiwa na madoa ya jasho na uchafu uliotoka kwa mkewe wakati wa safari ya usiku. Alikuwa akisali kimya kimya, mikono yake ikitetemeka kila mara daktari au muuguzi alipotoka kwenye chumba cha vipimo.

Ila kufikia saa sita mchana, Neema alirudishwa kwenye wodi ya dharura akiwa ametundikiwa dripu nyingine. Alikuwa amezinduka kidogo, lakini macho yake yalijaa unyonge na hofu kubwa kuliko wakati mwingine wowote. Alitazama pande zote za chumba kile cha hospitali, kisha macho yake yakatua kwa Juma aliyekuwa amesimama karibu na kitanda chake akimsikitikia.

Daktari bingwa alikuja akishika faili lenye majarida ya vipimo, uso wake ukiwa siriaz sana na wenye uzito mkubwa. Alimtazama Juma, kisha akamtazama Neema aliyekuwa akitoa ishara ya macho ya kuomba kitu.

Neema alijikaza, akainua mkono wake kwa tabu sana na kumshika Juma shati lake. Aligeuza kichwa chake kwa unyonge mkubwa, akajilazimisha kutoa sauti ya chini sana iliyokuwa ikikata: "Mume wangu... Juma... naomba ukae pembeni kidogo kule nje... nataka niongee na Salome peke yake kwanza... tafadhali mume wangu."

Juma alishtuka kidogo, akatazama daktari, kisha akamtazama mkewe kwa huruma. "Sawa mke wangu, usijali. Ngoja nitoke nje ili upumzike na uongee na mdogo wako. Mimi nipo hapa nje nakuombea," Juma alisema kwa upole, akambusu Neema kwenye paji la uso kabla ya kugeuka na kutoka nje ya chumba kile.

Daktari naye alielewa dharura ile; alirudi nyuma kidogo akitazama majibu kwenye faili, akatuacha mimi na dada yangu kwa sekunde kadhaa.

Mlango ulipofungwa, Neema alinigeukia. Macho yake yalijaa machozi yaliyomwagika mfululizo, yakitiririka mashavuni mwake yaliyokuwa yamebonyeza ndani. Alinitazama kwa huruma kubwa sana ambayo sitaisahau maisha yangu yote.

"Salome... mdogo wangu," Neema aliongea, sauti yake ikitetemeka kwa kilio cha ndani. "Nimekaa nalo sana hili jambo moyoni... nimeona leo nikwambie ukweli wote maana umenihangaikia sana mdogo wangu... kuanzia Kahama hadi sasa hivi tupo Bugando. Kiukweli tulikuwa tunapendana sana, na wewe ndio siri yangu yote."

Nilimsogelea karibu, nikashika mkono wake uliokuwa wa baridi na uliokonda sana. "Niambie dada yangu, mbona unalia hivyo? Kuna nini kimetokea mbona unanitisha?"

Neema alimeza mate kwa tabu, akajivuta karibu na sikio langu. "Salome... niliogopa kusema tangu mwanzo kwa sababu ya aibu... Shida yote hii haikuanza kwa ugonjwa wa kawaida. Ilianza pale nilipotumia zile product za kupunguza tumbo... kuna unga wa kahawia na vidonge nilikuwa nanywa kwa siri usiku wote ule."

Nilipigwa na bumbuazi, nikahisi kama chumba kizima kinarudi nyuma. "Dada! Product za kupunguza tumbo? Kwa siri?"

"Ndio mdogo wangu," Neema aliendelea kulia, huku akishikilia diaper aliyokuwa amevalishwa hospitalini hapo kwa sababu bado alikuwa anaharisha maji mfululizo. "Yule dada Aisha aliyeniuzia kule Instagram aliniambia nitaharisha siku 2 tu kutoa uchafu alafu nitakaa sawa... Ila haikuwa hivyo. Naharisha mpaka leo, utumbo wangu unakatika kwa maumivu, unateketea kwa ndani."

---

**Katika Episode Inayofuata (SURA YA 11: Namba ya Simu na Majibu ya Daktari):**
Mimi Salome ninajawa na hasira na maumivu makali baada ya kusikia ukweli huo. Neema ananipa namba ya simu ya yule mwanamke aliyemuuzia dawa hizo za sumu ili nimpigie. Wakati huohuo, daktari bingwa anarudi kitandani akiwa na majibu ya mwisho ya vipimo vya utumbo (*Endoscopy*). Je, utumbo wa Neema umepatwa na uharibifu kiasi gani, na daktari atatupa dokezo gani la kutisha? Usikose kufuatilia Sura ya 11!