✦ Matangazo ✦

📖 Story Tamu

Episode 5: USALITI WA MWANA

Sebule nzima ya Tino iligeuka kuwa uwanja wa vita vya maneno. Kelele za Asha na mashoga zake zilivuka ukuta na kuanza kuvutia majirani wa lile eneo la kishua, ambao walianza kusogea mlangoni mmoja baada ya mwingine kuchungulia nini kinaendelea kwenye lile ghorofa lililozoeleka kuwa na utulivu wa makaburi.

"Ati nini? Nyumba yenu?" Asha alicheka kwa sauti ya kigugumizi cha hasira, macho yakimtokata. Aligeuka kama simba na kumkamata Eddy shati lake lililokuwa wazi, akamvuta mbele kwa nguvu hadi Eddy akajikwaa na kuanguka karibu na miguu ya Cynthia. "Eddy! Simama hapa! Mwambie huyu pisi yako uliyoileta hapa kuwa mimi ni nani katika maisha yako! Na useme mbele ya hawa watu wote, huyu mwanamke unamjua?"

Eddy alikuwa anatetemeka kama mtu aliyepatwa na ugonjwa wa degedege. Alitazama upande wa mlangoni, akaona sura za majirani zikizidi kuongezeka, kisha akamtazama Asha ambae alikuwa ameshashika chupa ya bia tayari kuipasua kichwani kwake, na mwisho akamtazama Cynthia ambae alikuwa amesimama kwa maringo akitegemea kulindwa.

Eddy alijua fika kuwa Asha ndiye mwanamke aliyekuwa anajua siri zake zote za kifamilia, na ndiye mwanamke aliyekuwa na jeuri ya kumtibulia maisha yake. Akili ya kihuni ilimwambia lazima aokoe ngozi yake kwanza, hata kama ni kwa kumwaga mtu damu ya akili.

Eddy alinyanyuka, akajikuta anajifuta jasho, kisha akamnyoshea Cynthia kidole kilichokuwa kikitikisika kwa uoga.

"Mimi... mimi huyu dada namwona leo hapa! Simjui kabisa!" Eddy alifyatuka kwa sauti ya juu ili kila mtu asikie.

Cynthia alihisi kama amepigwa na radi ya mchana kweupe. Maringo yote yalimtoka mara moja. Macho yake makubwa na mazuri yalilegea kwa mshtuko, mdomo ukabaki wazi. "Eddy? Unasema nini? Mimi Cynthia wako... mke wako uliomwambia kuwa hii nyumba ni yako na unaishi peke yako? Eddy, unanikana mimi mbele ya hawa wahuni?"

"Wewe dada acha uongo na dharau!" Eddy alizidisha sauti, akijaribu kujitakatisha mbele ya Asha na umati wa majirani uliokuwa mlangoni. "Hapa sio kwangu, hapa ni kwa mshkaji wangu Tino! Mimi nimekuja kumtembelea Tino, nikakukuta wewe humu ndani sielewi umeingiaje! Usinitafutie matatizo na mke wangu Asha! Mimi na wewe hatujawahi hata kusalimiana, we malaya umetoka wapi?"

Maneno yale ya Eddy yalikuwa kama visu vilivyokuwa vinachoma moyo wa Cynthia. Kuitwa 'malaya' na mtu ambaye usiku wa jana tu alikuwa anamwambia yeye ndio malkia wa maisha yake, kulimfanya Cynthia aishiwe nguvu. Machozi yalianza kumtoka yakilowesha mashavu yake laini. Alijikuta akitazama chini kwa aibu kubwa, umati wa watu mlangoni ukianza kumzomea na kumnong'ona.

"Kumbe wezi wa waume za watu mkikamatwa mnajifanya wenye nyumba eh?" shoga mmoja wa Asha alifyatuka na kumsukuma Cynthia kwa mbele. Kile kigauni jekundu kilisukumwa kikatikisika, kikamfanya Cynthia alie kwa sauti ya chini, akijiziba uso kwa mikono yake mieupe. Alidhalilika kwa kiwango cha juu kabisa.

"Mtoe nje huyo malaya! Amefata nini kwenye ghorofa la watu? Mkati nguo zake!" Asha alipandisha mzuka na kuwasha moto, mashoga zake wakisogea mbele tayari kumvua Cynthia kile kigauni chake kifupi.

Cynthia alipiga magoti chini akilia na kuomba msamaha, akijua sasa hivi anaenda kutembezwa uchi mtaani kwa aibu ambayo hajawahi kuipata tangu azaliwe. Eddy alisimama pembeni akitazama ukuta, akijifanya haoni lolote ili tu asipoteze nafasi yake kwa Asha.

Huku dhoruba ikizidi kuwa kubwa na Cynthia akikaribia kuraruliwa nguo, Tino aliyekuwa amekaa kimya mda wote huo, alinyanyuka taratibu kutoka kwenye kochi. Alifunga kile kitabu chake cha biashara kwa sauti ya *mku!*, akasogea katikati ya ule umati, na kusimama mbele ya Cynthia aliyekuwa akilia chini.

---

**Katika Episode inayofata (Episode 6: Kauli ya Bosi):** Tino anaamua kuvunja ukimya mbele ya ule umati wa watu na kumkingia kifua Cynthia kwa kusema kauli itakayowaacha wote vinywa wazi. Je, Tino atasema nini ili kuokoa heshima ya huyu mwanamke aliyemdhau mwanzo? Usikose **Episode 6** hivi punde!