✦ Matangazo ✦

📖 Story Tamu

Episode 16: Kuzinduka kwa Mama Mwanahawa na Ukuta wa Kimya

Kumpambazuka kwa siku hiyo kulileta mwanga wa baridi ndani ya wodi ya hospitali. Nje ya dirisha, ndege walikuwa wakiimba kwa utulivu, lakini ndani ya moyo wa Mzee Juma kulikuwa na mshtuko mkubwa usio na kifani. Alikuwa amekaa kwenye kiti cha plastiki pembeni ya kitanda cha Mama Mwanahawa tangu saa kumi na moja za alfajiri, akiwa ameshika mikono yake miwili kifuani na kutazama kila mjongeo wa mke wake.

Mida ya saa mbili asubuhi, kope za Mama Mwanahawa zalianza kutetemeka taratibu. Alishusha pumzi ndefu ya uchovu, kisha akafumbua macho yake polepole.

Mwanga wa taa za hospitalini ulimstua kidogo. Macho yake yaliruka huku na huko kwenye kuta za wodi kabla ya kutua moja kwa moja usoni mwa Mzee Juma, aliyekuwa amekonda kwa hofu, macho yakiwa mekundu kwa kukosa usingizi na kilio cha usiku kucha.

"Mwanahawa... Mwanahawa mke wangu," Mzee Juma alinong'ona kwa sauti iliyovunjika, akijaribu kutabasamu huku machozi mapya yakimlenga. "Mungu ni mwema... umeamka mke wangu!"

Mzee Juma alinyoosha mkono wake ili kumshika mkono mke wake, lakini kitendo kilichofuata kilikuwa kama pigo la shoka kifuani mwake.

Mama Mwanahawa aliuondoa mkono wake taratibu kutoka kwenye kiganja cha Mzee Juma. Hakupiga kelele, hakulia, wala hakumuuliza swali lolote. Badala yake, aligeuza kichwa chake upande wa pili na kutazama ukuta wa wodi kwa kimya kizito—kimya cha dharau, maumivu na kukata tamaa kabisa.

"Mwanahawa... nakusihi unisikilize," Mzee Juma alijitupa chini kwa magoti pembeni ya kitanda. "Najua nimekosea sana mke wangu. Niliingia kwenye tamaa za uzeeni na kusahau utu na heshima yangu. Lakini Yule binti Loveness tayari amekamatwa na polisi usiku wa leo, na zile pesa zako za kikoba zimerudi zote hizi hapa! Yule binti alikuwa akinitishia na kurekodi mambo ya siri... Mwanahawa nisamehe mke wangu, usinifanyie kimya hiki!"

Mama Mwanahawa hakugeuka. Hakutoa hata sauti ya kuvuta pumzi kwa nguvu. Ukuta ule wa kimya uliendelea kusimama kati yao kama ghorofa la simenti. Kwa Mama Mwanahawa, picha ya video aliyoiona sebuleni usiku ule ilikuwa imefuta miaka thelathini ya heshima, upendo na uaminifu wao. Hakuumizwa tu na usaliti wa Mzee Juma, bali aliumizwa na jinsi mume wake alivyofikia hatua ya kupiga magoti na kuwa mtumwa wa binti mdogo mwenye umri wa watoto wao.

Daktari aliingia chumbani mda huo kufanya ukaguzi wa asubuhi. Alipomwona Mzee Juma akiwa amepiga magoti chini akilia na mke wake akiwa amempa mgongo, alielewa mazingira.

"Mzee Juma," Daktari alisema kwa utulivu wa kitaalamu. "Nilikwambia usiku wa kukia leo kwamba mgonjwa hatakiwi kupata presha ya aina yoyote. Utulivu wa akili ndio dawa yake kuu kwa sasa. Naomba utoke nje kidogo tumpe nafasi ya kupumzika."

Mzee Juma alijikokota kusimama. Alimwangalia mke wake kwa mara ya mwisho, lakini Mama Mwanahawa hakugeuka hata kidogo. Mzee Juma alitoka nje ya wodi akiwa ameinamisha kichwa, akijihisi kama mzoga unaotembea.

Alipofika nje ya jengo la hospitali, alimkuta Mwenyekiti Kijazi akimsubiri.

"Mzee Juma, hali ya Mama Mwanahawa ikoje?" Mwenyekiti aliuliza.

"Amezinduka Mwenyekiti..." Mzee Juma alijibu kwa sauti ya unyonge. "Lakini hataki hata kunitazama wala kuongea na mimi. Ananitazama kama vile mimi ni mgeni au mtu niliyekufa."

Mwenyekiti Kijazi alishusha pumzi. "Hilo lilikuwa la kutarajia Mzee Juma. Vidonda vya moyo haviponi kwa siku moja, hasa vilivyosababishwa na mtu uliyemwamini kwa miaka nenda rudi. Kwa sasa, tunatakiwa kwenda Kituo cha Polisi mara moja. Inspekta anahitaji maelezo yako rasmi ili jalada la Loveness likamilike na apelekwe mahakamani."

Mzee Juma alishtuka. Kumkabili Loveness uso kwa uso kituoni na kuandika maelezo ya aibu ile mbele ya polisi lilikuwa ni jaribio jingine gumu lililokuwa linamfata!

---

**Katika Episode 17 inayofuata: "Uso kwa Uso Kituo cha Polisi"**
*Mzee Juma anafika Kituo cha Polisi na kukutana na Loveness akiwa mahabusu. Loveness, akiwa amebanwa na pingu na kupoteza ujanja wake wote, anajaribu mbinu ya mwisho ya kumsihi Mzee Juma amsahihi ili asifungwe jela. Je, Mzee Juma atamhurumia au atasimama kidete kutafuta haki? Usikose!*