✦ Matangazo ✦

📖 Story Tamu

Episode 13: Kati ya Uhai na Mauti

Sauti ya breki za lori ilipasua ukimya wa barabara ya makutano ya kuelekea stendi ya mabasi ya Nyegezi. Anifa alihisi upepo mkali ukimpiga usoni, na mwili wake ukarushwa mita kadhaa pembeni ya barabara, akitua kwenye lundo la mchanga uliokuwa umeachwa na wajenzi.

Kila mtu aliyekuwa eneo lile alipiga kelele. "Daaah! Mrembo kachoka huyu, kashazidiwa na mawazo!" msamaria mmoja alipiga kelele akimkimbilia Anifa aliyekuwa amelala chali, damu kidogo ikimtoka kichwani na mguu wake wa kulia ukiwa umejipinda vibaya.

Mabegi yake ya gharama yalikuwa yamesambaratika barabarani. Nguo za hariri na viatu vya bei mbaya vilikuwa vimejaa vumbi na damu. Hakuna aliyeamini kuwa huyu ndiye yule malkia aliyekuwa akitamba kwenye mitandao ya kijamii siku chache zilizopita.

"Mpelekeni Hospitali ya Mkoa haraka!" sauti ya askari wa usalama barabarani iliamuru.

Gari la wagonjwa (Ambulance) lilifika kwa haraka. Lilipowasili hospitalini, nesi aliyekuwa zamu alipiga kelele. "Jamani! Huyu si mke wa zamani wa Dr. Hassan? Haraka, iteni Dr. Hassan yuko wodini!"

Hassan alikuwa akimaliza kumfanyia upasuaji mgonjwa mwingine wakati nesi alipoingia kwa hofu. "Dokta, kuna dharura. Anifa ameletwa, amepata ajali mbaya ya kugongwa na lori."

Hassan alihisi ganzi mwilini. Alimtazama Ashura aliyekuwa amekuja kumletea chai ya jioni. Ashura alimshika mkono kwa upole. "Mume wangu, nenda. Wewe ni daktari, na huyo ni binadamu anayehitaji msaada wako sasa hivi. Usiangalie yaliyopita."

Hassan aliingia chumba cha dharura. Alimkuta Anifa akiwa hajitambui, akitapatapa kwa maumivu huku akitaja jina lake kwa sauti ya chini, "Hassan... nisamehe... Hassan..."

Hassan alifanya kazi kwa saa nne mfululizo. Alishona majeraha, alitibu mguu uliovunjika, na kuhakikisha damu inasimama. Kila alipokuwa akimgusa Anifa, alikumbuka ngozi hiyo hiyo alivyokuwa akiipaka mafuta ya gharama wakati wa furaha yao. Lakini sasa, ngozi hiyo ilikuwa imejaa makovu na vumbi.

Baada ya saa kadhaa, Anifa alifumbua macho kwa shida. Alimuona Hassan akiwa amesimama pembeni yake, amevaa nguo za upasuaji zilizojaa damu.

"Hassan... bado unaniokoa?" Anifa alinong'ona kwa sauti dhaifu sana.

"Anifa, mimi ni daktari. Kazi yangu ni kuokoa maisha," Hassan alijibu kwa sauti kavu, isiyo na hisia za mapenzi lakini yenye utu mwingi. "Umeshapata nafuu, lakini mguu wako utachukua muda mrefu kupona. Utalazimika kutumia magongo kwa miezi kadhaa."

Anifa alilia. Uzuri wake uliokuwa "mtaji" wake sasa ulikuwa umechafuka. Mguu wake mmoja sasa ulikuwa umefungwa bandeji nzito (P.O.P). Alijitazama kwenye kioo kidogo kilichokuwa pembeni na kuona uso wake ukiwa na makovu ya kioo cha lori.

"Uzuri wangu umeenda, Hassan... sina kitu tena," Anifa alisema kwa uchungu.

"Uzuri wa sura ni kama maua, Anifa. Hukauka," Hassan alisema huku akivua glavu zake. "Ulipaswa kuthamini uzuri wa roho na utu. Sasa hivi huna marafiki, huna utajiri wa Mzee Mvule, na mimi nina maisha yangu mapya. Utakapopona, itabidi uanze maisha upya, peke yako."

Hassan alitoka nje na kumkumbatia Ashura aliyekuwa akimsubiri kwa uvumilivu koridoni. Anifa alibaki kwenye kitanda cha hospitali, akitazama dari nyeupe, akijua kuwa safari yake ya majuto sasa ndiyo imeanza rasmi.

---
**Je, Anifa atakubali kuishi maisha ya ulemavu na umaskini? Na Bi Husna atachukua hatua gani akisikia Anifa yuko hospitalini? Usikose Sehemu ya 14.**