✦ Matangazo ✦

📖 Story Tamu

Episode 1: Mkia wa Kenge

Siku hiyo Juma aliamka saa tano asubuhi, lakini akajigeuza tena kitandani mpaka saa sita. Alikuwa anatumia mbinu yake ya kijeshi kuwa **siyo kila anayeamka saa sita mchana ni tajiri, wengine wanapunguza tu saa za kuteseka** wakiwa macho.

Alipoamua kunyanyuka, alienda mbele ya kioo cha duka la Mangi kilichopasuka. Alijitazama akagundua amepauka hadi anafanana na ukuta wa shule ya msingi iliyojengwa enzi za mkoloni. Alijikagua mifukoni; akakuta vumbi, kokoto mbili, na risti ya duka la mwaka juzi.

Juma alishusha pumzi ndefu na kujisemea, **"Kama huna gari, huna nyumba, huna simu na huna hela, tofauti yako na kenge ni mkia tu."** Alijigusa nyuma ya suruali yake ya "kadeti" iliyofubaa, akashukuru Mungu angalau mkia ulikuwa bado haujachomoza, japo mwendo wake ulishaanza kufanana na mjusi aliyebanwa na mlango.

Aliamua kuwa liwalo na liwe; lazima aende mjini Dar es Salaam. Alichukua mswaki wake mmoja uliopoteza nywele upande wa kushoto akauweka mfukoni. Alijua fika kuwa **dalili nyingine ya umasikini ni kusafiri na mswaki tu**, lakini hakuwa na namna. Alianza kupiga hatua kuelekea stendi huku akipita katikati ya kundi la mifugo ya jirani yake.

---

**Kionjo cha Episode 2:** Akiwa anapita katikati ya kundi la ng’ombe, ghafla mmoja anatoa sauti "Mooo!", Juma anasimama na kumuuliza, "Kwani unajua siri zangu?" Usikose **Ep 2: "Kikao cha Ng’ombe."**