✦ Matangazo ✦

📖 Story Tamu

Episode 25: UKWELI CHINI YA KIAPO

Macho ya daktari yalikuwa makali kama kisu cha upasuaji, yakisubiri jibu kutoka kwa Baraka. Ndani ya ile ofisi ndogo, sauti ya feni ya dari ilikuwa ikizunguka kwa dharura, ikiongeza shinikizo kwenye akili ya Baraka. Alitazama mikono yake iliyokuwa na mivimbe ya jasho la sokoni, kisha akakumbuka sura ya Loveness iliyopauka kule chumba cha dharura.

"Daktari..." Sauti ya Baraka ilivunjika, na machozi yalianza kumtiririka laivu. Alijiachia kutoka kwenye kiti na kupiga magoti mbele ya meza ya daktari. "Nakuomba unisaidie... usituite polisi. Ni kweli, Loveness sio mke wangu wa ndoa. Yeye ni binamu yangu wa damu. Baba yake na baba yangu ni mtu na kaka yake."

Daktari alishusha pumzi ndefu, akisogeza miwani yake juu. Sio mara yake ya kwanza kukutana na visa vya ajabu vya kijamii, lakini dharura ya kibaolojia iliyokuwa mbele yake ilikuwa kubwa mno.

"Tulipendana tangu tukiwa mkoani, daktari," Baraka aliendelea kufunguka kwa uchungu, akitetemeka. "Wazazi wametufukuza, tumekimbilia Manzese kisha Mbagala kujificha... Hatuna mtu yeyote mjini hapa. Nakuomba uokoe maisha yake, mimi niko tayari kufanya lolote."

Daktari alimshika Baraka begani na kumnyanyua. "Simama kijana. Mimi ni tabibu, jukumu langu la kwanza ni kuokoa maisha, sio kuhukumu maadili yenu. Lakini sayansi haidanganyi. Hiyo hitilafu ya kijenetiki niliyokuambia ni hatari. Kinga ya mwili ya Loveness inazalisha sumu kupiga vita kiumbe kilichopo tumboni kwa sababu damu zenu zimekaribiana mno. Mimba hii haitakaa itengeneze mtoto kamili, na kadiri inavyokua, inasababisha mishipa ya uzazi ya Loveness kuvuja damu ya ndani na inaenda kufeli figo zake. Ili Loveness aishi, maamuzi ni mamoja tu..."

Daktari alimtazama Baraka kwa dhati ya kitaalamu. "Inabidi tufanye upasuaji wa dharura wa kutoa hii mimba (*Therapeutic Abortion*) sasa hivi kabla sumu haijasambaa mwilini mwake. Ukikataa, ndani ya saa ishirini na nne zijazo, utakuwa na maiti mbili mkononi mwako."

Baraka alihisi kama amepigwa na nyundo ya chuma kichwani. Mtoto wao... kile kiumbe walichokilinda na kukikimbilia Mbagala, kilikuwa kinaenda kutolewa ili kuokoa maisha ya Loveness. "Fanya... fanya upasuaji huo daktari. Maisha ya Loveness ndio kila kitu kwangu," Baraka alijibu kwa sauti ya chini kabisa, akisaini fomu za dharura za kuruhusu matibabu.

Wakati hayo yakiendelea ofisini, kule mapokezi ya chumba cha dharura, muuguzi mmoja wa kike aliyeitwa Sister Grace alikuwa akiandika majina ya wagonjwa kwenye daftari kuu. Alipofika kwenye faili la Loveness na kuona jina la ukoo na jina la Baraka aliyemleta kama mdhamini, alistuka.

Alichomoa simu yake ya mkononi kwa dharura, akafungua group la WhatsApp la ukoo wao wa kule mkoani. Siku mbili zilizopita, kulikuwa na tangazo zito lililosambazwa na picha za Baraka na Loveness zikisomeka: *"Yeyote atakayewaona vijana hawa wawili waliokimbia laana ya ukoo, atoe taarifa haraka. Kuna zawadi ya fedha na wazee wa mila wako njiani kuja Dar es Salaam."*

Sister Grace alitazama picha kwenye simu, akalinganisha na majina yaliyopo kwenye faili, kisha akajisemea moyoni: *"Ni wao! Hawa ndio wale watoto waliovunja miiko ya ukoo!"* Bila kupoteza sekunde, alibonyeza namba ya simu ya kiongozi wa ukoo uliosambaza tangazo hilo ili kutoa siri ya mahali walipo.

---

**Utangulizi wa Episode Inayofuata:**
Katika **Episode 26: Mtego wa Hospitalini**, wakati Loveness akiwa ameingizwa chumba cha upasuaji kutoa ule ujauzito uliotaka kumuua, wazee wa mila kutoka mkoani wakiongozana na baadhi ya ndugu wa karibu wa Dar es Salaam wanafika hospitalini hapo kwa kasi baada ya kupewa siri na yule muuguzi. Baraka anajikuta amezingirwa kwenye korido za hospitali huku Loveness akiwa bado hajazinduka kutoka kwenye kisu cha daktari. Je, Baraka atafanya nini kuwalinda sasa? Usikose sehemu inayofuata!